Friday, April 4, 2014

SIMBA KUIVAA KAGERA SUGAR VPL.

MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 kesho (Aprili 5 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo Kagera Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbeya City ambayo itakuwa mgeni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah Kibaden ipo katika mkakati wa kukwepa kushuka daraja. Keshokutwa (Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Coastal na Mgambo Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT na Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na Mtibwa Sugar (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam). Raundi hiyo itakamilika Aprili 9 mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.



NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU UJAO
Ni ipi kati ya timu za Mwadui na Stand United, zote za Shinyanga itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao itajulikana kesho (Aprili 5 mwaka huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu. Mwadui yenye pointi 28 ndiyo inayoongoza, na itacheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Nayo Stand United yenye pointi 26 itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Mechi nyingine zitakuwa kati ya Pamba na Kanembwa JKT itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi Mara na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Timu ambazo tayari zimepanda daraja kutoka FDL kucheza VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi Morogoro ya kundi B.



No comments:

Post a Comment