Tuesday, April 29, 2014

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa ya Mikoa-RCL msimu wa 2013-2014 inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vitakavyokuwa na timu tisa kila kimoja. Katika taarifa taarifa ya TFF iliyotumwa kwa vyombo vya habari, imedai kuwa mechi za michuano hiyo zitachezwa kwa mkondo mmoja katika vituo ambavyo ni Mbeya, Morogoro na Shinyanga. Mshindi katika kila kituo cha ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Juni 2 mwaka huu atakuwa amekata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi Daraja la Kwanza-FDL kwa msimu wa 2014-2015. Wakati huohuo timu ya taifa ya Malawi inatarajiwa kuwasili nchini Mei mosi kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars utakaochezwa Mei 4 mwaka huu katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mchezo huo utakuwa mahsusi kwa ajili ya Stars inayonolewa na kocha mpya Mart Nooij kujiandaa na mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Zimbabwe utakaochezwa kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.


No comments:

Post a Comment