Tuesday, May 27, 2014

ROAD TO BRAZIL: DIEGO COSTA HATARINI KUZIKOSA FAINALI ZA MICHUANO YA KOMBE LA DUNIA.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Hispania mzaliwa wa Brazil, Diego Costa yuko hatarini kuzikosa fainali za Kombe la dunia baada ya madaktari kuonya jana kuwa majeruhi ya msuli yanaweza kumlazimisha kupumzika kwa wiki mbili. Costa mwenye umri wa miaka 25 alitolewa uwanjani baada ya kupita dakika tisa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kati ya timu yake ya Atletico Madrid na Real Madrid Jumamosi iliyopita baada ya kufanya matibabu ya dharura ya kuchanika msuli. Daktari Pedro Guillen ambaye ni mkuu wa kliniki ya Cemtro ambapo wachezaji wa Hispania hufanyiwa vipimo vyao, amesema Costa alikuwa bado hajapona majeraha yake hata kabla ya mchezo huo uliopita. Guillen aliendelea kudai kuwa nyota huyo anahitaji mapumziko ya wiki mbili, na anaweza kwenda Brazil lakini itategemea na jinsi atakavyoendelea. Kocha wa Hispania Vicente del Bosque amemua kusogeza mbele muda wa kutaja kikosi chake cha mwisho ili kufuatilia hali ya Costa na wachezaji wengine wa Atletico na Real Madrid baada ya fainali hiyo iliyopita. Hispania ambao ni mwabingwa wa Ulaya na mabingwa watetezi wa Kombe la dunia litakalofanyika nchini Brazil mwezi ujao wanatarajia kuanza kampeni yao dhidi ya Uholanzi Juni 13 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment