Tuesday, May 27, 2014

ROAD TO BRAZIL: MAJERUHI YAZIDI KUIANDAMA CAMEROON.

NAHODHA wa timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o alipumzishwa wakati hofu ya majeruhi kuelekea katika Kombe la Dunia ikizidi kupanda wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Macedonia uliochezwa huko Austria. Mshambuliaji huyo wa Chelsea aliwekwa benchi kwasababu ya matatizo ya goti aliyonayo lakini Cameroon ilikumbwa na balaa lingine baada ya mshambuliaji wake mkongwe kulazimika kutolewa nje katika mchezo huo uliochezwa jana. Pierre Webo mwenye umri wa miaka 32 aliumia bega wakati akifunga bao la kuongoza kwa timu hiyo hatua ambayo ilimfanya kutolewa nje na nafasi kuchukuliwa na Eric Maxim Choupo-Moting aliyeongeza bao la pili dakika za mwisho. Webo na Eto’o wanaingia katika orodha ndefu ya wachezaji majeruhi ambao waliachwa katika mechi hiyo ili waweze kupona sawasawa akiwemo golikipa Charles Itandje, bekli Jean-Armel Kana-Biyik na viungo Edgar Salli, Jean Makoun na Stephen Mbia. Mechi hiyo ilichezwa pamoja na kutofikiwa makubaliano kati ya wachezaji na maofisa wa Shirikisho la Soka la Cameroon juu ya kiasi gani cha fedha watapewa kutoka kwa mdhamini mazungumzo ambayo yanatarajiwa kumalizika mwishoni mwa wiki hii. Cameroon wataanza kampeni yao kwa kuivaa Mexico Juni 13 huko Natal lakini bado wana mechi za kujipima nguvu dhidi ya Paraguay, ujerumani na Moldova kabla ya kwenda huko Brazil.

No comments:

Post a Comment