KATIKA kuelekea katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwezi ujao kumekuwa na matukio mbalimbali yanayoendelea yakiwemo makocha wa timu za taifa kuanza kutoa orodha ya wachezaji watakaowatumia katika michuano hiyo. Mbali na hayo vyombo vya habari mbalimbali duniani navyo vimekuwa vikijipanga ili kuhakikisha wanafikisha taarifa sahihi kwa wateja wao ambao hawatakuwepo huko Brazil kushuhudia michuano hiyo. Kwa kuonyesha umuhimu wa michuano hiyo ulivyo shirika la habari nchini Uingereza BBC nalo limetangaza kikosi kazi kwa ajili ya michuano hiyo ambacho kitaongozwa na Thierry Henry na Rio Ferdinand. Mtangazaji kiongozi wa luninga Gary Lineker atakuwa sambamba na Ferdinand ambaye ni nahodha wa zamani wa Uingereza, Henry ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 1998 na kiungo wa zamani wa Uholanzi ambaye ni kocha wa sasa wa AC Milan Clarence Seedorf. Kazi kubwa ya nyota hayo safari hii itakuwa sio kutoka jasho kama ilivyokuwa wakati wakicheza bali ni kuchambua kwa makini mechi zote 64 zitakazochezwa katika michuano hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani kote.
No comments:
Post a Comment