KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Al Markhiya ya Qatar, Mwinyi Kazimoto amewasili nchini kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mechi ya kufuzu michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe. Kazimoto ametua nchini jana ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka nchini TFF iliyotumwa leo mchezaji huyo ameshaondoka kwenda Tukuyu, mkoani Mbeya tayari kujiunga na timu hiyo iliyoweka kambi yake huko chini ya kocha Mart Nooij. Stars ilicheza mchezo wa kirafiki wa maandalizi dhidi ya Malawi Jumapili iliyopita ambapo walitoka sare ya bila ya kufungana mchezo ambao ulikuwa sehemu ya maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo dhidi ya Zimbabwe. Wakati huohuo, Shirikisho la Soka la Afrika-CAF limeteua waamuzi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC kuchezesha mchezo kati ya timu ya taifa ya Tanzania-Ngorongoro Heroes na Nigeria. Mchezo huo wa mchujo kusaka tiketi ya kucheza fainali za 19 za vijana chini ya umri wa miaka 20 zinazotarajiwa kufanyika nchini Senegal mwakani, utachezwa mwishoni mwa wiki hii katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Waamuzi hao wataongozwa na Jean-Jacques Ndala Ngambo atakayesaidiwa na Oliver Safari Kabene, Nabina Blaise Sebutu na Mupemba Ignace Nkongolo. Kamishna wa mechi hiyo namba 37 ni Poiret Antoine Ralph Danny kutoka Shelisheli.
No comments:
Post a Comment