Wednesday, May 21, 2014

KILELE CHA MICHUANO YA BEACH SOCCER JUMAPILI.

MICHUANO ya mpira wa miguu ya ufukweni-beach soccer inatarajiwa kufikia kileleni Mei 25 mwaka huu kwa mchezo wa fainali utakaozikutanisha timu za Taasisi ya Teknologia Dar es Salaam-DIT na Chuo cha Elimu ya Biashara-CBE kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini hapa. Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini-TFF Boniface Wambura mgeni rasmi katika fainali hiyo itakayoanza asubuhi anatarajiwa kuwa rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi. Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni. Tanzania inatarajiwa kushiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.

No comments:

Post a Comment