KLABU ya AC Milan imethibitisha kuwa kiungo Sulley Muntari amesaini mkataba mpya utakaomuweka hapo mpaka Juni mwaka 2016. Kufuatia kutimuliwa kwa Clarence Seedorf na nafasi kuchukuliwa na Filippo Inzaghi kama kocha wa timu hiyo, klabu hiyo imeamua kumbakisha kiungo huyo wa kimataifa wa Ghana kuelekea maandalizi yao ya msimu ujao. Kiungo huyo alijiunga na Milan akitokea kwa mahasimu wao wa jiji Inter kwa mkopo Januari mwaka 2012 kabla kusaini mkataba wa kudumu ilipofika kipindi cha usajili majira ya kiangazi mwaka huo huo. Muntari mwenye umri wa miaka 29 ambaye amewaji kucheza katika vilabu vya Udinese na Portsmouth hakuwa na msimu mzuri aliposaini mkataba wa kudumu hata hivyo msimu uliopita amekuwa akipata namba ya kudumu kutokana na kiwango chake kuimarika. Kiwango chake kimeishawishi timu hiyo kumuongeza mkataba mwingine wa miaka miwili zaidi. Kwasasa mchezaji huyo yuko na kikosi cha timu ya taifa ya Ghana nchini Brazil kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia na wanatarajiwa kupambana na Ujerumani katika mchezo wao pili utakaochezwa Jumamosi hii.
No comments:
Post a Comment