SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limeeleza kusikitishwa kwake na taarifa za mashabiki wa soka nchini Nigeria kufa kutokana na mlipuko wakati wakitizama mechi za Kombe la Dunia. Rais wa FIFA Sepp Blatter ameelezea tukio hilo kama la kutisha katika mchezo soka huku akihubiri kuwa mchezo wa soka unatakiwa kutumika kama chombo cha kuwaunganisha watu. Blatter aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa ni jambo la kutisha kusikia taarifa za vifo na majeruhi nchini Nigeria wakati mashabiki wakitizama Kombe la Dunia na kuongeza kuwa soka linatakiwa kuwaunganisha watu na sio kuwagawa. Watu wapatao 14 wanaaminika kuuwawa katika mlipuko uliotokea eneo la Tsamiya Lilo huko Damaturu katika jimbo la Yobe ambapo inaaminika kuwa mlipuko huo ulitokea kutoka katika baiskeli iliyopaki pembeni ya eneo hilo. Mwaka 2010 watu wapatao 74 waliuawa katika milipuko miwili tofauti iliyotokea jijini Kampala, Uganda wakati wakitizama mechi za Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment