MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uingereza, Wayne Rooney amesisitiza kuwa anafurahi kucheza mahali popote uwanjani baada ya kutupwa katika wingi ya kushoto katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ecuador jana. Nyota huyo alifunga bao la kusawazisha katika kipindi cha kwanza wakati Uingereza walipotoa sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo uliochezwa jijini Florida na hivyo kumaliza ukame wake wa kucheza mechi za kimataifa nne bila bao. Hodgson aliamua kumuondoa Rooney katika nafasi yake ambayo ilichukuliwa na mchezaji mpya wa Liverpool Rickie Lambert kama mshambuliaji wa kati baada ya nyota huyo wa Manchester United kupondwa kutokana na kiwango chake katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Peru wiki iliyopita. Lakini Rooney ambaye aliwahi kulalamika kuchezeshwa nyuma ya Robin van Persie wakati wa msimu wa mwisho wa Sir Alex Ferguson Old Trafford, amesema yuko tayari kucheza popote kwa timu yake ya taifa katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil. Rooney amesema huwa anafurahia kuitumikia nchi yake hivyo haijalishi atapangwa mahali gani kwani hilo ni jukumu la kocha atakavoona yeye.
No comments:
Post a Comment