Thursday, June 19, 2014

KOMBE LA DUNIA 2014: MARADONA AIZUSHIA FIFA KUMZUIA KUINGIA MARACANA.

NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona amedai kuwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA lilimfungia kutohudhuria mechi ya timu ya taifa ya nchi yake dhidi ya Bosnia Jumapili liyopita. Maradona ambaye ameichezea Argentina mechi 91, amedai kuwa alizuiwa kuingia katika Uwanja wa Maracana kutizama mechi hiyo ambayo Argentina walishinda kwa mabao 2-1 na kulazimika kuingalia katika luninga akiwa hotelini kwake. Maradona mwenye umri wa miaka 53 ambaye alikuwepo katika kikosi cha nchi hiyo kilichonyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1986, amesema alizuiwa kwenda katika mchezo huo hivyo aliamua kurudi na kutizama kipindi cha pili katika luninga. Nguli amesema alifanya kila alichoweza ili kujaribu kuingia kutizama mchezo huo lakini ilishindikana, ni mategemeo yake kuwa suala hilo litakwisha ili aweze kuingia katika mechi zilizosalia za nchi yake. Hata hivyo FIFA wenyewe walikanusha taarifa hizo za kumzuia Maradona kuhudhuria mechi hiyo ya ufunguzi ya nchi yake na kudai kuwa kulikuwa hakuna taarifa yoyote ya tukio lililomhusu Maradona. Mkuu wa habari wa FIFA Delia Fischer amesema hakupata taarifa yoyote ya tukio lililomhusisha nguli huyo wa zamani wa soka ambaye alikuwa ana kibali cha kama mwandishi wa luninga ya Venezuela.

No comments:

Post a Comment