MENEJA wa klabu ya Manchester City, Manuel Pellegrini amesema kwasasa bado wako sokoni wakitafuta wachezaji wapya wa kuwasajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kiweze kutetea taji lake msimu ujao. Pellegrini tayari ameshamsajili kiungo wa Brazil Fernando kutoka Porto, beki wa kimataifa wa Ufaransa Bacary Sagna kutoka Arsenal na kipa Willy Caballero kutoka klabu yake ya zamani ya Malaga lakini bado hajatosheka na wachezaji hao aliowapata. Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea katika mchezo wao kirafiki dhidi ya Sporting Kansas City huko Marekani, Pellegrini amesema hadhani kama kikosi chake kimekamilika hivyo kuna uwezekano wa kuongeza mchezaji mmoja au zaidi. Mipango ya Pellegrini kutaka kumnunua mshambuliaji wa Real Madrid Alvaro Negredo inaweza kuwa imebadilika baada ya mchezaji huyo kuvunjika mguu katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Ijumaa iliyopita dhidi ya klabu ya Hearts ya Scotland. City watachuana na AC Milan, Liverpool na Olympiakos Piraeus katika ziara yao nchini Marekani kabla ya kurejea kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa msimu mpya wa ligi kugombea ngao ya hisani dhidi ya mabingwa wa Kombe la FA Arsenal Agosti 10 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment