Monday, July 21, 2014

BOLT KUSHIRIKI MASHINDANO MAALUMU YA RIO DE JANEIRO.

MWANARIADHA nyota wa mbio fupi anayeshikilia rekodi ya duniani, Usain Bolt anatarajiwa kuelekea jijini Rio de Janeiro kushiriki mashindano maalumu yam bio za mita 100 kabla ya kuelekea jijini Glasgow, Scotland kwa ajili ya michuano ya Jumuiya ya Madola. Shindano hilo litakalofanyika katika ufukwe wa Copacabana Agosti 14 mwaka huu ndio litakamilisha ratiba ya Bolt kwa mwaka huu wa 2014 hivyo kumaanisha kuwa hataweza kukutana na nyota wa Marekani ambaye amerejea katika makali yake Justin Gatlin mpaka mwaka 2015. Gatlin mwenye umri wa miaka 32 ameshinda mashindano 11 mfululizo ya mbio za mita 100 na mawili yam bio za mita 200 kwa mwaka huu. Ratiba ya Bolt pia inajumuisha mbio za mita 100 zitakazofanyika nchini Poland Agosti 23 mwaka huu na mashindano ya Diamond League yatakayofanyika jijini Zurich Agosti 28 mwaka huu. Gatlin ambaye alirejea uwanjani baada ya kutumikia adhabu ya kufungiwa miaka minne kwa kosa kutumia madawa ya kuongeza nguvu mwaka 2010, hatapewa mwaliko wa kushindano na Bolt katika mashindano ya Zurich kwasababu ya sera zao za kutowaalika wanariadha ambao wamewahi kufungiwa kwa kosa hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

No comments:

Post a Comment