Thursday, July 24, 2014

HUENDA CAS IKAMPUNGUZIA ADHABU SUAREZ.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez anaweza kupunguziwa adhabu yake ya kufungiwa miezi minne, hivyo kumpa nafasi ya kucheza kucheza mechi ya kwanza ya La Liga akiwa na timu yake mpya ya Barcelona katika msimu wa mwaka 2014-2015. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 alifungiwa kucheza mechi tisa za kimataifa huku akifungiwa miezi minne kutojishughulisha na mambo ya soka na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kosa la kumng’ata beki wa Italia Giorgio Chiellini wakati wa michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika nchini Brazil. Baada ya rufani yake kupinga adhabu hiyo kukataliwa na FIFA, Suarez alikamilisha usajili wake kwenda Barcelona kwa ada ya euro milioni 88 ingawa klabu hiyo ilishindwa kumtambulisha rasmi kutokana na adhabu hiyo. Barcelona waliamua kupeleka rufani yao katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo-CAS ambapo kumekuwa na tetesi kuwa adhabu hiyo inaweza kupunguzwa. Tetesi hizo zimedai kuwa kuna uwezekano mkubwa CAS wakapunguza au kuondoa kabisa adhabu ya miezi minne na kubakisha ile ya kutumikia mechi tisa za kimataifa na faini ya euro 82,000 alizotozwa.

No comments:

Post a Comment