RAIS wa Shirikisho la Soka nchini-TFF, Jamal Malinzi amekemea vikali wimbi la upangaji matokeo mechi za kimataifa lililoibuka huko katika nchi za bara la Asia ambapo sasa inasemekana limeshafika mpaka Afrika. Malinzi ametoa kauli hiyo katika futari aliyoandaa jana kwa wadau mbalimbali wa michezo kikiwemo kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys katika ofisi za shirikisho hilo, Dar es Salaam. Malinzi amesema ana uhakika kuwa balaa hilo la upangaji mechi za kimataifa limeingia Afrika huku wanaofanya shughuli hizo wakiwashawishi viongozi, makocha na hata wachezaji ili matokeo yapatikane wanavyotaka wao. Malinzi amesema sio suala la kuficha tena kuhusu janga hilo na kuwaomba wadau na viongozi wa dini waliokuwepo katika shughuli hiyo kuungana ili kuwakemea vijana wao kuhusu suala hilo. Mojawapo ya viongozi mbalimbali waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Ramadhani Madabida, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF enzi hizo ikiitwa FAT Said El Maamry na viongozi mbalimbali wa timu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la kwanza Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment