Thursday, July 24, 2014

RATIBA YA LA LIGA YATOKA, EL CLASICO KATI YA BARCELONA NA REAL MADRID ITAKUWA OCTOBA NA MACHI.

TIMU mahasimu katika Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga, Barcelona na Real Madrid zinatarajiwa kukutana mwezi Octoba na Machi baada ya ratiba ya ligi msimu wa 2014-2015 kutangazwa mapema leo. Shirikisho la Soka la Hispania-RFEF lilithibitisha kuwa mchezo wa kwanza kati mahasimu hao ambao pia hujulikana kama Clasico Madrid watakuwa wenyeji wa Barcelona katika Uwanja wa Santiago Bernabeu Octoba 26 huku ule wa marudiano ukichezwa katika Uwanja wa Camp Nou Machi 22 mwakani. Ratiba hiyo inamaanisha mshambuliaji mpya wa Barcelona Luis Suarez anaweza asiruhusiwe kucheza mechi ya kwanza ya Octoba kama adhabu yake ya kufungiwa miezi minne haitapunguzwa wakati nyota wapya wa Madrid Toni Kroos wa Ujerumani na James Rodriguez wao wanaweza kucheza mechi yao ya kwanza ya El Clasico. Hata hivyo kabla ya mechi hiyo timu zote mbili zitaanza kampeni yao ya ligi kwa kucheza nyumbani ambapo Barcelona wataikaribisha Elche huku Madrid wakiwa wenyeji wa Cordoba mwishoni mwa wiki ya Agosti 23 na 24. Kwa upande wa mabingwa watetezi wa La Liga Atletico Madrid wao wataanza kampeni zao ugenini kwa kuivaa Rayo Vallecano huku Sevilla akiwa wenyeji wa Valencia, Levante wakipambana nyumbani na Villareal na Malaga wakicheza na Athletic Bilbao.

No comments:

Post a Comment