WINGA mahiri wa klabu ya Arsenal, Theo Walcott anatarajiwa kukosa mwanzo wa msimu kutokana na majeruhi ya goti yanayomsumbua lakini anatarajiw akurejea tena uwanjani mwishoni mwa Agosti mwaka huu. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 25 aliumia goti lake la kushoto katika mchezo wa Kombe la FA mzunguko wa tatu dhidi ya Tottenham Hotspurs Januari mwaka huu. Majeruhi hayo yalipelekea nyota huyo kukosa msimu uliobakia wa ligi sambamba na michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika hivi karibuni nchini Brazil. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger amesema anategemea Walcott kurejea tena katika mazoezi rasmi mwishoni mwa Agosti kutokana na majeruhi yake kuendelea kupona vyema. Walcott amekuwa kama ana bahati mbaya na michuano ya Kombe la Dunia kwani mwaka 2010 pia aliachwa na kocha wa kipindi hicho Fabio Capello kutokana na majeruhi aliyopata katika kipindi cha mwisho wa msimu.
No comments:
Post a Comment