KLABU ya Arsenal imepangwa kucheza na Besiktas katika ratiba ya mtoano ya kuingia katika makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopangwa jijini Nyon, Uswis. Arsenal wanaonolewa Arsene Wenger mara ya mwisho kutinga hatua ya timu 16 bora katika michuano hiyo ilikuwa msimu wa 2009-2010 na watatakiwa kufanya vyema zaidi msimu huu lakini bado wana safari ndefu ya kufikia huko kwani itabidi waitoe klabu hiyo Uturuki kwanza kabla ya kuingia katika makundi. Kwa upande mwingine klabu ya Napoli ya Italia inayonolewa na Rafael Benitez nayo itakuwa na kibarua kizito baada ya kupangwa kucheza na washiriki wa La Liga Athletic Bilbao. Napoli wamekuwa wakishiriki michuano hiyo kwa miaka mitatu mfululizo huku wakitolewa katika hatua ya makundi msimu uliopita huku wenzao Bilbao wakiwa wametokea katika michuano hiyo mara moja pekee wakati walipotolewa katika hatua ya makundi msimu wa 1998-1999. Timu zingine ni Lille ya Ufaransa itakayopambana na FC Porto ya Ureno, Bayer Leverkusen ya Ujerumani itachuana na FC Copenhagen ya Denmark huku Standard Liege ikichuana na Warusi Zenit Saint-Petersburg. Mechi za mkondo wa kwanza zinatarajiwa kuchezwa Agosti 19 na 20 huku mechi za marudiano zikitarajiw akuchezwa Agosti 26 na 27 ambapo washindi 10 watajiunga na timu 22 zilizofuzu moja kwa moja katika hatua za makundi.
No comments:
Post a Comment