USHINDI wa bao 1-0 iliyopata klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC dhidi ya Zamalek ya Misri umeihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Matokeo hayo yameifanya Vita na ndugu zao TP Mazembe kuvuka hatua hiyo katika kundi A wakiwa wamefikisha alama 10 huku wakiwa wamebakisha mechi moja baina yao wenyewe itakayochezwa jijini Kinshasa ili kuamua nani atakuwa kiongozi wa kundi. Zamalek mabingwa mara tano wa michuano hiyo sasa watakwaana na Al-Hilal ya Sudan ambao wote wana alama nne ambapo mshindi kati yao anaweza kupata nafasi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho. Kwa upande wa kundi B CS Sfaxien ya Tunisia na Entene Setif ya Algeria ndio waliojihakikishia nafasi ya kutinga hatua hiyo na kuziacha timu za Esperance na Al-Ahly Benghazi zikipigana mechi ya mwisho kulinda heshima zao. Bingwa wa michuano hiyo ambayo inaandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF atakunja kitita cha dola milioni 1.5 na tiketi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika baadae mwaka huu nchini Morocco.
No comments:
Post a Comment