Monday, August 4, 2014

MECHI ZA KUFUZU AFCON 2015: TANZANIA, KENYA OUT, UGANDA YATAKATA.

MECHI za kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika zilizofanyika mwishoni mwa wiki zimekuwa na habari mbaya kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki baada ya Tanzania na Kenya kushindwa kusonga mbele wakati majirani zao Uganda wakifanikiwa kutinga hatua ya makundi. Kenya waliokuwa wamewakaribisha Lesotho walijikuta waking’olewa bila kutegemea baada ya kung’ang’aniwa sare ya bila ya kufungana katika mchezo uliochezwa jijini Nairobi, matokeo ambayo yalipelekea kutolewa kwa tofauti ya 1-0. Matokeo hayo yamepelekea Shirikisho la Soka nchini humo-KFF kufukuza benchi lote la ufundi lililokuwa likiongozwa na kocha mzaliwa wa Ubelgiji Adel Amrouche. Katika mchezo huo ambao Kenya walionyesha kuumudu vyema waliwatumia nyota wake wote akiwemo Victor Wanyama anayesakanata kabumbu katika klabu ya Southampton ya Uingereza na MacDonald Mariga anayecheza soka ya kulipwa nchini Italia. Lesotho sasa watacheza mechi zao za kufuzu katika kundi C wakiwa sambamba na timu za Angola, Burkina Faso na Gabon wakati Uganda wao watakuwa katika kundi E sambamba na timu za Ghana, Guinea na Togo. Msumbiji ambao wao waliiondosha Tanzania kwa jumla ya mabao 4-3 watakuwa katika kundi F sambamba na timu za Cape Verde, Niger na Zambia. Jumla ya nchi 28 zinatarajiwa kushindana katika makundi saba kati ya Septemba, Octoba na Novemba ili kuamua nchi zitakazoungana na wenyeji Morocco kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika mwakani. Washindi wawili katika kila makundi ndio watakaofuzu kushiriki michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment