MASHINDANO ya Jumuiya ya Madola yamemalizika jana jijini Glasgow, Scotland huku mji huo ukimiminiwa sifa kem kem kwa kuandaa mashindano yaliyofana. Sifa hizo zilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Mashindano ya Jumuiya ya Madola Mike Hooper kwa kuandaa mashindano hayo. Baada ya siku 11 ya matukio mbali mbali ya michezo 17 hatimaye sherehe za ufungaji wa mashindano zilifanyika katika uwanja wa Hampden Park jana usiku huku wenyeji wa mashindano hayo Scotland wakimaliza wakiwa nafasi ya nne kwa kunyakua medali za dhahabu 19. Uingereza ndio wameibuka kidedea kwa mara ya kwanza tangu miaka 28 iliyopita kwa kunyakuwa medali 58 za dhahabu wakifuatiwa na Australia katika nafasi ya pili wakiwa na medali 49 za dhahabu na Canada wako katika nafasi ya tatu kwa kuchukua medali 32 za dhahabu. Kwa upande wa Afrika, nchi ya Afrika Kusini ndio imeongoza kwa kuwa katika nafasi ya saba baada ya kuchukua medali 13 za dhahabu, wakifuatiwa na Nigeria wenye medali 11 za dhahabu huku Kenya wakifuatia kwa karibu kwa kuchukua medali 10 za dhahabu. Katika mashindano hayo Tanzania ambayo iliwakilishwa na wanamichezo 39 hawakuambulia chochote hivyo kupelekea kurudi nyumbani wakiwa mikono mitupu.
No comments:
Post a Comment