MECHI za hatua ya makundi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon mwakani zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo ambapo nchi 28 zitakuwa zikitafuta nafasi 15 kwa ajili ya kujiunga na mwenyeji Morocco katika michuano hiyo Januari mwakani. Kuelekea katika michuano hiyo siala kubwa lililokuwa limetawala ni juu ya viwanja vitakavyotumika kwa baadhi ya mechi kutoka na wasiwasi wa ugonjwa hatari wa Ebola. Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF limeziamuru nchi za Guinea na Sierra Leone kuhamisha mechi zao za nyumbani katika viwanja huru kwasababu ya mlipuko wa ugonjwa huo kwenye nchi hizo. Guinea wao wamehamishia mechi yao ya kundi E dhidi ya Togo huko Casablanca nchini Morocco huku wakikabiliwa na majeruhi kadhaa katika kikosi chao akiwemo Florentin Pogba ambaye ni kaka mkubwa wa nyota wa kimataifa wa Ufaransa Paul Pogba. Pogba alipata majeruhi wakati klabu ya ya Saint Etienne ilipochabangwa kwa mabao 5-0 na mabingwa wa Ufaransa Paris Saint Germain Jumapili iliyopita. Guinea pia itawakosa kiungo wa Lorient Abdoulaye Sadio Diallo na mshambuliaji wa Lyon Mohamed Lamine Yattara wakati wapinzani wao Togo wao watakuwa na ahueni baada ya mshambuliaji Emmanuel Adebayor kurejea katika majukumu ya kimataifa baada ya kukosekana kwa miezi 18. Mechi nyingine itakayochezwa baadae leo utakuwa mchezo wa kundi E utakaozikutanisha Senegal na Misri jijini Dakar. Washindi wawili kutoka katika kila kundi watafuzu na kuungana na Morocco katika fainali za Afcon Januari mwakani.
No comments:
Post a Comment