MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Nicolas Anelka amejiunga katika klabu ya Mumbai City inayoshiriki ligi mpya ya soka nchini India inayojulikana kama Indian Super League. Nyota huyo wa zamani wa vilabu vya Arsenal na Real Madrid alitimuliwa katika timu ya West Bromwich Albion kutokana na utovu wa nidhamu. Kutimuliwa kwake kulikuja baada ya kufungiwa na kutozwa faini na Chama cha Soka cha Uingereza kwa kuonyesha ishara ya salamu za Kinazi wakati wa mchezo. Anelka mwenye umri wa miaka 35 alithibitisha taarifa hizo za kujiunga na Mumbai City katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter na kueleza furaha yake kucheza katika ligi ya huko. Ligi hiyo itakayochukua muda wa wiki 10 inatarajiwa kuanza mwezi ujao huku lengo lake kubwa likiwa ni kuongeza msisimko wa soka nchini humo.
No comments:
Post a Comment