Friday, September 19, 2014

DEBUCHY NJE WIKI SITA.

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema Mathieu Debuchy atakaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu. Beki huyo wa kimataifa wa Ufaransa ambaye alitolewa nje kwa machela katika mchezo dhidi ya Manchester City Jumamosi iliyopita anaweza kukosekana kwa miezi mitatu kama itahitajika kufanyiwa upasuaji. Wenger alithibitisha hilo na kudai kuwa matokeo zaidi watayajua katika siku chache zijazo baada ya kufanyiwa vipimo zaidi kuonyesha jinsi eneo hilo lilivyoathirika. Calum Chambers mwenye umri wa miaka 19 anatarajiwa kuchukua nafasi ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 katika mchezo wa kesho dhidi ya Aston Villa. Debuchy ambaye alijiunga na Arsenal akitokea Newcastle United Julai mwaka huu amecheza katika mechi zote saba za timu hiyo msimu huu ukiwemo mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Manchester City. Beki mwingine kinda Hector Bellerin mwenye umri wa miaka 19 ndio aliyeingia kuxcheza nafasi ya upande wa kulia katika mchezo wa Jumanne waliofungwa na Borussia Dortmund kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments:

Post a Comment