MABINGWA watetezi Hispania na Uingereza zimeanza vyema kampeni zao za kufuzu michuano ya Ulaya mwakani baada ya kuchinda mechi zao za jana. Hispania ambao wako kundi C wao walikuwa wakicheza na vibonde Macedonia ambapo walifanikiwa kuwagaragaza kwa jumla ya mabao 5-1 yaliyofungwa na Paco Alcacer, Sergio Busquets, Sergio Ramos, David Silva na Pedro. Kwa upande wa Uingereza wao walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Switzerland katika mchezo wa kundi E mabao ambayo yalifungwa na mshambuliaji mpya wa klabu ya Arsenal Danny Welbeck. Katika michezo ya kundi G wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia 2018, Urusi nao walionyesha makali yao kwa kuigaragaza Liechtenstein kwa mabao 4-0 huku Sweden wao waking’ang’aniwa sare ya bao 1-1 na Austria. Mzunguko wa kwanza wa mechi za kufuzu unatarajiwa kukamilika leo ambapo viwanja nane vitawaka moto barani humo. Jumla ya timu 23 zinatarajiwa kufuzu kutoka katika makundi tisa na mtoano na kujiunga moja kwa moja na wenyeji Ufaransa katika michuano ya Ulaya mwaka 2016 ambayo kwa mara ya kwanza itashirikisha timu 24 badala ya 16 kama ilivyozoeleka.
No comments:
Post a Comment