Friday, September 26, 2014

KIONGOZI WA QATAR ATAMBA NCHI HIYO KUANDAA KOMBE LA DUNIA BORA ZAIDI KUWAHI KUTOKEA.

KIONGOZI wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani jana amesema taifa hilo la Ghuba litaandaa moja ya michuano bora kabisa katika historia ya Kombe la Dunia wakati watakapokuwa wenyeji wa michuano hiyo mwaka 2022. Qatar na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwasasa wako chini ya shinikizo kali la kuondoa michuano hiyo ya mwaka 2022 kutoka katika nchi hiyo huku kukizungukwa na tuhuma za rushwa katika kupata nafasi hiyo. Ligi kubwa barani Ulaya pia zinapinga wazo la kuhamisha michuano hiyo kutoka kiangazi mpaka majira ya baridi ili kuepuka joto kali katika miezi ya kiangazi nchini Qatar. Akihojiwa na CNN kiongozi huyo amesema watu wanapaswa kuelewa kuwa Qatar ni mzabuni bora na anaweza kuandaa michuano bora kabisa kuwahi kutokea katika historia. Al-Thani aliendelea kudai kuwa tatizo la watu wengi hawataki kukubali kuwa nchi ndogo ya Kiarabu inaweza kuandaa michuano mikubwa kama hiyo. Kiongozi huyo aliendelea kutamba kuwa Qatar ina uwezo wa kuandaa michuano hiyo wakati wa kiangazi kama walivyoahidi tena bila tatizo lolote na kama wakiamua kubadili na kupeleka majira ya baridi pia wako tayari.

No comments:

Post a Comment