Thursday, September 25, 2014

LIVERPOOL YAINGIA MATATANI UEFA.

KLABU ya Liverpool ni moja ya vilabu kadhaa vinavyotarajiwa kufanyiwa uchunguzi kama wamekiuka Sheria ya Matumizi ya Fedha-FFP. Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA vilabu vyote barani humo vinapaswa kuweka kikomo cha hasara kutofikia paundi milioni 35.4 kwa misimu miwili. Kuna adhabu hutolewa kwa wasiotimiza masharti hayo ambapo Manchester City tayari wameshakumbana nayo kwa kutozwa faini na kuwekewa kiwango cha matumizi katika usajili na kupunguziwa idadi ya wachezaji katika kikosi chake Mei mwaka huu. Lakini pamoja na kupata hasara ya paundi milioni 49.8 katika msimu wa mwaka 2012-2013 na paundi milioni 41 msimu wa mwaka 2011-2012, Liverpool wana uhakika wanaweza kuvuka kikwazo hicho bila adhabu. Liverpool sambamba na vilabu vya Monaco, Inter Milan na AS Roma ambazo zote hazikushiriki michuano ya Ulaya msimu uliopita tarayi zimepeleka taarifa za akaunti zao Bodi ya Udhibiti wa Fedha ya Klabu-CFCB lakini kuna uwezekano wa kuagizwa kupelekea maelezo zaidi kuhusu fedha hizo. Msimu uliopita vilabu 76 viliingia katika uchunguzi wa FFP lakini vilabu tisa pekee ndio vilipewa adhabu kwa kukiuka sheria hiyo.

No comments:

Post a Comment