BEKI wa zamani wa Manchester United, Phil Neville amedai kuwa klabu hiyo inahitaji kutumia tena kitita cha paundi milioni 100 kwa ajili ya kununua wachezaji kabla ya kuanza kushindania taji la Ligi Kuu nchini Uingereza. United ilitandikwa kwa mabao 5-3 na Leicester City Jumamosi iliyopita lakini Neville amesema hakushangazwa na matokeo hayo. Neville mwenye umri wa miaka 37 amesema anajua kuwa United wametumia kitita cha paundi 150 katika usajili uliopita lakini anafikiri vipindi vingine viwili vya usajili ambavyo watahitajika kutumia kiasi kama hicho cha pesa kabla ya kuanza kufikiria kushionda taji. Meneja mpya wa United Louis van Gaal alitumia kitita cha paundi milioni 150 kuwasajili viungo Angel Di Maria, Ander Herrera na Daley Blind pamoja na mabeki Marcos Rojo na Luke Shaw wakati Mshambuliaji Radamel Falcao yeye alichukuliwa kw amkopo wa paundi milioni sita. Neville amesema United kwasasa wanapaswa kuangalia uwezekano wa kupata beki mzuri wa kati sambamba na kiungo mkabaji au mchezaji anayeweza kucheza nafasi ya kiungo wa kati. Tyler Blackett mwenye umri wa miaka 20 ndio amekuwa akicheza nafasi ya beki wa kati katika mechi tano za Ligi Kuu za United msimu huu lakini alionekana kuzidiwa na kasi ya Leicester na kutolewa nje.
No comments:
Post a Comment