Thursday, September 11, 2014

MAYWEATHER ATANGAZA KUSTAAFU NGUMI MWAKANI.

BONDIA mahiri Floyd Mayweather amesema amedhamiria kupata mapambano mawili zaidi baada ya pambano lake la marudiano na Marcos Maidan litakalofanyika jijini Las Vegas Jumamosi hii kabla ya kuamua kustaafu rasmi mchezo huo mwaka 2015. Hata hivyo, bondia huyo mwenye umri wa miaka 37 amezima taarifa kuwa yuko katika mazungumzo na bondia nguli wa Philippine Manny Pacquiao. Mayweather ambaye hajawahi kupigwa katika mapambano 46 ya ngumi za kulipwa aliyopigana, alimtandika kwa alama Maidana ambaye ni raia wa Argentina katika pambano lao la kwanza lililochezwa Mei mwaka huu. Akihojiwa Mayweather ambaye anashikilia ubingwa wa dunia uzani wa welterweight na light-middleweight alithibitisha kauli yake hiyo ya kustaafu huku akikana promota wake kufanya mazungumzo na Pacquiao. Bondia huyo aliendelea kudai kuwa hajui yatakayotokea huko mbele lakini anadhani kwasasa promota wa Pacquiao anajaribu kuuza tiketi kwa ajili ya pambano la bondia huyo dhidi ya Chris Algieri litakalofanyika Novemba 22 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment