MCHEZAJI wa soka nchini Uganda Fahad Musana ameanguka na kufariki muda mchache baada ya Frank Lampard kufunga bao kusawazisha katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uingereza kati ya Manchester City na Chelsea. Kifo cha Musana mwenye umri wa miaka 24 kimekuja kwa mshtuko hususani baada ya beki huyo kucheza mechi yote katika ya klabu yake ya Simba iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Entebe FC katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Uganda uliofanyika katika Uwanja wa Nakivubo. Kwa mujibu wa kocha wa Simba Fred Kajoba, Musana pia alifanya mazoezi na timu siku ya jana asubuhi katika viwanja vya Bombo na hakuonyesha tatizo lolote. Shirikisho la Soka la Uganda-FUFA lilituma taarifa za kifo hicho cha ghafla jana usiku ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Barracks iliyopo huko Bombo kwa ajili taratibu za mazishi. Shuhuda aliyekuwepo eneo ambalo Musana alikuwa akitazama mechi hiyo amesema mchezaji huyo alikuwa akifurahia mchezo huo mpaka ilipofikia hatua ya Lampard aliposawazisha ndipo alipoanguka ghafla ya kukimbizwa hospitali ya Jeshi ya Bombo. Inaarifiwa kuwa mbali na kupenda kucheza kamari, Musana alikuwa shabiki wa kutupwa wa Chelsea na alikuwa yuko tayari kufanya lolote kwa ajili ya timu hiyo. Mashabiki wa soka la Uingereza nchini Uganda wamekuwa wakipata matukio katika miaka ya karibuni ambapo mwaka jana mshabiki wa klabu ya Arsenal aliripotiwa kupoteza nyumba baada ya kuweka kamari kwamba timu hiyo ingeifunga Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu lakini matokeo yake wakafungwa bao 1-0.
No comments:
Post a Comment