KOCHA wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque amesisitiza kuwa haitawezekana Lionel Messi amudu kucheza kwa kiwango chake cha juu muda wote lakini anadhani nyota huyo wa Barcelona atabaki kuwa mchezaji wa kipekee. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina amepitia katika wakati mgumu msimu uliopita mpaka baadhi ya wadau kudai kuwa makali ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 tayari yamekwisha. Hata hivyo, Del Bosque amesisitiza kuwa ni jambo la kawaida kwa mchezaji kama Messi kucheza chini ya kiwango kwa baadhi ya nyakati lakini anafikiri bado ni mmoja ya washambuliaji bora waliopo hivi sasa. Del Bosque amesema ni jambo gumu mara zote kuwa katika kiwango cha Messi hivyo ijulikane kuwa hata wachezaji bora kama yeye na Cristiano Ronaldo huwa nao wanapitia hali hiyo. Toka msimu umeanza Messi ameifungia Barcelona mabao mawili katika mchezo walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Elche kabla ya kutengeneza bao la ushindi katika mchezo wao dhidi ya Villarreal ambao walishinda bao 1-0.
No comments:
Post a Comment