KIUNGO mkongwe wa kimataifa wa Italia, Andrea Pirlo amesema bado ana nia ya kuendelea kuitumikia timu yake ya taifa pamoja na kudokeza baada ya michuano ya Kombe la Dunia kuwa muda wake wa kustaafu umefika. Pirlo mwenye umri wa miaka 35 anayetumikia klabu ya Juventus amesema amezungumza na kocha mpya wa Italia Antonio Conte na amemuuliza kama anaweza kuwa tayari kuitumikia nchi hiyo na amemwambi kwamba bado anaweza. Mkongwe huyo amesema ni uamuzi mgumu aliochukua kwani alikuwa akitaka kustaafu soka la kimataifa lakini Conte alipochukua nafasi ya ukocha alimuomba amsaidie na anajisikia furaha kufanya hivyo huku akiwa na matumaini ya kufanya makubwa chini yake. Conte amewahi kumfundisha Pirlo kwa misimu mitatu wakati akiwa bado hajaondoka Juventus na kufanikiwa kushinda mataji matatu mfululizo ya Serie A kabla ya kuamua kuchukua mikoba ya Cesare Prandelli aliyeachia ngazi baada ya nchi hiyo kushindwa kuvuka hatua ya makundi katika Kombe la Dunia. Mechi ya kwanza Conte akiwa kama kocha wa Italia ilichezwa Alhamisi iliyopita ambapo waliitandika Uholanzi kwa mabao 2-0 huko Bari.
No comments:
Post a Comment