Tuesday, September 9, 2014

UHOLANZI WATANGAZA KUMNYIMA KURA BLATTER KATIKA UCHAGUZI WA FIFA MWAKANI.

CHAMA cha Soka cha Uholanzi-KNVB kimedai kutompigia kura Sepp Blatter ambaye amethibitisha kugombea tena urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kipindi cha tano. Rais wa KNVB Michael van Praag aliwaambia waandishi wa habari kuhusu msimamo wao huo jana lakini akakiri kuwa haoni kama kuna mtu anayeweza kumng’oa Blatter katika nafasi hiyo. Uholanzi mara kadhaa wamekuwa wakimpinga Blatter mwenye umri wa miaka 78 ambaye alichukua madaraka hayo kutoka kwa Joao Havelange mwaka 1998. Katika mkutano mkuu wa FIFA uliofanyika nchini Brazil kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia, KNVB ilimpasha Blatter kuwa anatakiwa astaafu huku wakimtaka kuwajibika kutoka kashfa mbalimbali zilizolikumba shirikisho hilo. Lakini Blatter anaonekana bado kutaka kuendelea kukomalia nafasi hiyo kwa kipindi kingine kitakachomaliza mwaka 2019 akiwa na umri wa zaidi ya miaka 83, baada ya rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA Michel Platini kuweka wazi kuwa hatagombea kiti hicho. Praag amesema bahati mbaya Platini amekataa kugombea kwani ndiye mtu pekee ambaye angeweza kusimama na Blatter.

No comments:

Post a Comment