Friday, September 12, 2014

WAPINZANI WA BLATTER WANAPASWA KUTANGAZA NIA NA SIO KUKOSOA UAMUZI WAKE - WATZKE.

OFISA mkuu wa klabu ya Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amesema wapinzani wa rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter wanapaswa kugombea nafasi hiyo dhidi yake badala ya kukosoa uamuzi wake wa kuamua kutetea kiti chake. Watzke pia aliliambia shirika la habari la Reuters katika mahoajiano kuwa itakuwa bora kama michuano ya Kombe la Dunia 2022 haitaandaliwa na Qatar. Blatter mwenye umri wa miaka 78 ambaye ameingoza FIFA toka mwaka 1998 alitangaza wiki hii kuwa atagombea kipindi kingine cha tano pamoja na tuhuma za rushwa zinazodaiwa kufanyika wakati wa kuipa Qatar uenyeji wa kuandaa Kombe la Dunia 2022. Rais huyo ambaye atakuwa anatimiza miaka 79 wakati wa upigaji kura katika uchaguzi wa Juni mwakani alitangaza wiki hii kuwa atagombea tena katika mkutano wa Soccerex uliofanyika jijini Manchester. Watzke amesema watu wanapaswa kuwa waangalifu wanapokosoa na kama kuna watu popote wanaodhani muhula wa tano ni kipindi kirefu au umri wake umekuwa mkubwa kushikilia nafasi hiyo basi wanapaswa kugombea dhidi yake na sio kusemasema maneno pembeni. Mpinzani pekee ambaye alikuwa akitegemewa kutoka upinzani wa karibu kwa Blatter, rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA Michel Platini ameamua kutogombea nafasi hiyo mwakani.



No comments:

Post a Comment