WAZIRI wa michezo wa Afrika Kusini, Fikile Mbalula amesema leo kuwa nchi hiyo haiku tayari kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika Januari mwakani kama Morocco watajivua uenyeji kwasababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Imeripotiwa kuwa Shirikisho la Soka la Afrika-CAF lilizifuata Afrika Kusini, Ghana na nchi zingine tano kuelekea katika mkutano wao wa Novemba 2 kuamua mustakabali wa michuano hiyo. Lakini waziri huyo aliviambia vyombo vya habari vya nchi hiyo kuwa hawako tayari kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwani wana majukumu ya kuhakikisha wanasaidia kupambana na kuutokomeza ugonjwa huo ambao mpaka sasa umeshaua zaidi ya watu 4,500. Mbalula amesema hata wakati kabla suala hilo halijapelekwa katika bunge la nchi hiyo kujadiliwa jibu lilikuwa ni hapana kwani walikuwa hawana uwezo wa kutosha kwasasa kuandaa michuano hiyo. Afrika Kusini imeweza kuandaa michuano hiyo mara mbili kwa dharura, baada ya kuchukua nafasi ya Kenya mwaka 1996 walioshindwa kwa kukosa fedha na Libya mwaka jana kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
No comments:
Post a Comment