KLABU ya Real Madrid imethibitisha katika mtandao wake kuwa Gareth Bale amepata majeruhi ya paja hivyo kuweka wasiwasi wa kukosekana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool na mchezo wa La Liga dhidi ya Barcelona mwishoni mwa wiki hii. Bale aliondolewa katika benchi la wachezaji wa akiba wakati wa ushindi wa mabao 5-0 iliyopata Madrid dhidi ya Levante Jumamosi iliyopita na sasa anategemewa kukaa nje kwa muda. Katika taarifa yake Madrid imedai kuwa baada ya nyota huyo kufanyiwa vipimo aligundulika kupata majeruhi hayo katika mguu wake wa kulia. Bale amekuwa mchezaji muhimu wa Madrid toka ajiunge nao akitokea Tottenham Hotspurs katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka jana. Nyota huyo wa kimataifa wa Wales amefunga mabao 22 katika mechi 44 alizocheza katika mashindano yote msimu uliopita ikiwemo bao moja katika mchezo wa fainali ya Ligi ya mabingwa msimu uliopita ambapo walishinda mabao 4-1 dhidi ya Atletico Madrid. Masimu huu Bale tayari ameshafunga mabao matano katika mechi 12 za mashindano yote alizocheza.

No comments:
Post a Comment