Sunday, October 5, 2014

CHAMBERS AITWA KIKOSI CHA UINGEREZA KUZIBA NAFASI YA STONES.

CHIPUKIZI Calum Chambers ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha timu ya taifa ya Uingereza baada ya John Stones kulazimika kujitoa kutokana na majeruhi. Beki huyo wa klabu ya Arsenal, alikuwa ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa cha vijana chini ya umri wa miaka 21 kinachonolewa na Gareth Southgate kwa ajili ya mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwakani dhidi ya Croatia. Lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 sasa amejumuishwa katika kikosi cha Roy Hodgson kuelekea katika mechi za kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya San Marino na Estonia. Stones amejitoa kufuatia kuumia kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Manchester United ambao Everton walitandikwa kwa mabao 2-1. Kutokana na hilo Chama cha Soka cha Uingereza-FA kilitoa taarifa ya Hodgson kumchukua Chambers kutoka katika kikosi cha Southgate. Uingereza itakwaana na San Marino katika Uwanja wa Wembley Alhamisi hii kabla ya kuivaa Estonia huko Tallinn siku tatu baadae.

No comments:

Post a Comment