KOCHA wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte amesema ni juu ya kikosi chake kuamua kuipa kipaumbele timu hiyo kwa ajili ya mashabiki wao. Toka waliponyakuwa taji la Kombe la Dunia mwaka 2006, Italia imeshindwa kuvuka hatua ya makundi katika michuano hiyo iliyofanyika Afrika Kusini na Brazil. Conte ana matumaini atawaburudisha mashabiki na kutengeneza vichwa vya habari wakati Italia itakapokuwa mwenyeji wa Azerbaijan katika mchezo wa kundi H wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 utakafanyika huko Palermo baadae leo. Kocha huyo amesema mechi za kufuzu ni muhimu kwao hivyo wanahitaji mashabiki wawaunge mkono badala ya kuwazomea na ili kufanikisha hilo wanapaswa kushinda mchezo wa leo sambamba na kucheza soka safi litakalowaburudisha. Conte alichukua mikoba ya kuinoa Italia kutoka kwa Cesare Prandelli aliyetimuliwa baada ya kufanya vibaya katika Kombe la Dunia nchini Brazil.

No comments:
Post a Comment