Wednesday, October 8, 2014

FERGUSON ALITAKA KUNIPA JEZI NAMBA 7 BADALA YA BECKHAM - KEANE.

NAHODHA wa zamani wa klabu ya Manchester United, Roy Keane amedai alipewa ofa ya kupewa jezi maarufu ya namba saba katika klabu hiyo na aliyekuwa meneja Sir Alex Ferguson ili kuzia David Beckham kuipata jezi hiyo. Keane ambaye aliondoka United mwaka 2005 baada ya kuitumikia kwa miaka kadhaa alibainisha hayo katika kitabu chake kipya kiitwacho The Second Half ambacho kimeanza kuuzwa katika mitaa mbalimbali ya jiji la Manchester kabla ya muda wake halisi wa kutoka. Kwa mujibu wa Keane baada ya nguli wa zamani wa Ufaransa Eric Cantona kuondoka klabuni hapo mwaka 1997, Ferguson alikuwa hataki kumpa Beckham jezi hiyo ambayo imevaliwa na manguli kama Bryan Robson na George Best huku baadae Cristiano Ronaldo akiivaa. Katika kitabu hicho Keane amekaririwa akidai kuwa katika United namba saba ni namba ya kipekee hivyo wakati Cantona alipondoka kulikuwa na mjadala nani apewe jezi ya namba hiyo tena. Keane aliendelea kudai kuwa Ferguson alimvuta ofisini kwake na kumwambia anataka aivae jezi namba saba kwani anajua Beckham ataitaka nay eye hakupenda kumpa lakini alikataa ombi hilo. Hata hivyo baada ya Keane kukataa, Beckham alikuja kupewa jezi hiyo baada ya kuelewana vyema na Ferguson mpaka uhusiano wao ulipokuja kuyumba mwishoni na kupelekea Beckham kutimkia Real Madrid ya Hispania. Keane aliitumikia United kwa kipindi cha miaka 12, nane kati ya hiyo akiwa nahodha na kufanikiwa kushinda mataji saba ya Ligi Kuu, manne ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.

No comments:

Post a Comment