Tuesday, October 14, 2014

KUONA MECHI YA YANGA NA SIMBA 7,000.

SHIRIKISHO la Soka nchini-TFF limetangaza viingilio vya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha mahasimu Yanga na Simba ambapo kiingilio cha chini kabisa kitakuwa ni shilingi 7,000. Mchezo baina ya timu hizo unatarajiw akuchezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Taarifa hiyo ya TFF iliyotumwa katika mtandao imeendelea kudai kuwa mashabiki watakaolipa kiingilio hicho ni wale watakaokaa katika viti vya rangi bluu na kijani ambavyo jumla yake ni viti 36,693 katika uwanja huo wenye jumla ya viti 57,558. Viingilio vingine katika mchezo ni shilingi 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, 20,000 kwa jukwaa la VIP B na C wakati VIP A kiingilio kitakuwa shilingi 30,000. Tiketi zitakazotumika kwenye mechi hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa jana kupitia mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam. Mechi hiyo namba 27 itakayochezeshwa na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na John Kanyenye na Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Washabiki wanatakiwa kununua tiketi mapema, kwani hazitauzwa uwanjani siku ya mechi.


No comments:

Post a Comment