Saturday, October 18, 2014

NYOTA WA SIERRA LEONE ASIMAMISHWA NA KLABU YAKE HUKO UGIRIKI BAADA YA KUTOKA KUTUMIKIA TIMU YAKE YA TAIFA.

KLABU ya PAS Lamia ya Ugiriki limemtaka mchezaji wa kimataifa wa Sierra Leone John Kamara kutofanya mazoezi au kucheza katika klabu hiyo kwa muda wa wiki tatu kwa hofu ya ugonjwa wa Ebola. Kamara alirejea nchini Ugiriki baada ya kuitumikia nchi yake katika michezo miwili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Cameroon. Klabu hiyo ilimuambia Kamara kuwa uamuzi huo umekuja kufuatia ushauri wa wizara ya afya ya nchi hiyo. Kamara amesema Lamia wamemwambia apumzike kwa siku 15 mpaka 21 ili waweze kuona maendeleo yake baada ya kutoka Afrika kuitumikia nchi yake. Sierra Leone walilazimika kuandaa mchezo wao wa nyumbani nchini Cameroon katika jiji la Younde kwasababu ya nchi hiyo kufungiwa kucheza nyumbani na Shirikisho la Soka la Afrika-CAF kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Kamara amesema wakati wako nchini Cameroon walikuwa wakichekiwa joto la mwili kila asubuhi na jioni na aliwaweka wazi Lamia kuwa wamfanyie vipimo vyovyote kwani anajua hajaambukizwa Ebola lakini hawakutaka hivyo inabidi aheshimu uamuzi wao.

No comments:

Post a Comment