RAIS wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Michel Platini jana ameunga mkono upigaji kura upya wa kutafuta mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2022 kama kutakuwa na ushahidi wa ufisadi wakati Qatar ikipewa uenyeji wa michuano hiyo. Platini ambaye pamoja na makamu wake waliipigia kura Qatar kuwa mwenyeji wa michuano hiyo amesema alifanya hivyo bila ya ushawishi kutoka popote na kama itagundulika kulikuwa na vimelea vya ufisadi katika zoezi hilo basi ataunga mkono upigaji mpya wa kura. Toka kuchaguliwa kwa Qatar kumekuwa na mjadala wa kubadilisha michuano hiyo kupelekea majira ya baridi kutokana na joto kali linalokuwepo katika nchi hiyo majira ya kiangazi. Mbali na hayo lakini tuhuma za rushwa zimekuwa zikiizonga nchi hiyo pamoja na Urusi waliopewa haki ya kuandaa michuano ya mwaka 2018 hatua ambayo imepelekea mpaka kuundwa tume kuchukunguza suala hilo. Wakili wa kujitegemea wa Marekani Michael Garcia ndio aliyepewa jukumu hilo na tayari ameshawasilisha ripoti kamili ya uchunguzi wake ambapo Shiikisho la Soka Duniani-FIFA limesema litaufanyia kazi kwa siri.

No comments:
Post a Comment