Monday, November 17, 2014

AFCON 2015: SABA ZAFUZU, NANE ZINGINE KUJULIKANA JUMATANO.

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika-Afcon iliendelea tena wiki iliyopita ambapo timu saba ambazo ni Afrika Kusini, Burkina Faso, Gabon, Cameroon, Cape Verde, Tunisia na Senegal ziliungana na Algeria katika nchi zilifuzu michuano hiyo itakayochezwa mwakani huko Guinea ya Ikweta. Katika kundi A Afrika Kusini walifuzu bada ya kuichabanga Sudan kwa mabao 2-1 huku Nigeria ambao nao wako katika kundi hilo wakifufua matumaini yao kwa kuifunga Congo Brazzaville kwa mabao 2-0. Afrika kusini wamefikisha alama 11 katika mechi tano walizocheza wakifuatia na Nigeria na Congo ambao wote wana alama saba huku Sudan wakiwa na alama tatu na kama Nigeria wakiifunga Bafana Bafana Jumatano hii nao watakuwa wamejihakikishia nafasi hiyo. Kundi B Algeria pamoja na kufuzu waliendelea ubabe kwa kuichapa Ethiopia kwa mabao 3-1 wakati Malawi wao waligaragaza Mali kwa mabao 2-0 na kuweka hai matumaini yao ya kufuzu. Kundi C Burkina Faso na Gabon zilijihakikishia nafasi yao ya kushiriki michuano hiyo ambapo Burkina Faso wao waliichapa Lesotho kwa bao 1-0 huku Gabon wao wakitoa sare ya bila ya kufungana na Angola. Wengine waliofuzu na makundi wanayotoka ni Cape Verde kutoka kundi F ambao waliifunga Niger kwa mabao 3-0 wkati kundi G Tunisia nao walizosonga mbele pamoja na sare ya bila kufungana na Botswana huku Senegal nao wakiwaadhibu Misri nyumbani kwao wa bao 1-0.

No comments:

Post a Comment