MSHAMBULIAJI mkongwe wa kimataifa wa Italia, Francesco Totti amebainisha kuwa angependa kuwa kocha wa AS Roma mara atakapoamua kutundika daruga zake. Totti mwenye umri wa miaka 38, ametumia muda wake wote wa kucheza soka akiwa na Roma na kufunga mabao 293 katika mechi 718 huku karibuni akiwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mkubwa kufunga bao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiulizwa kama angependa kufuata nyayo za Roberto Mancini sambamba na mchezaji mwenzake wa zamani Vincenzo Montella na Pep Guardiola za kuja kuwa kocha, Totti alikiri itakuwa ngumu kukataa nafasi hiyo. Totti amesema angependa kuinoa Roma mara atakapoamua kutundika daruga zake na kuongeza pengine anaweza kuanza na timu za watoto lakini kutokana na uzoefu wake hadhani kama itamchukua kipindi kirefu kabla ya kufundisha timu ya wakubwa.
No comments:
Post a Comment