MCHEZO wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 kati ya Italia na Croatia uliingiwa na dosari mara mbili jana wakati miwako iliporushwa uwanjani na polisi kuvamia jukwaani kutuliza ghasia za mashabiki. Mchezo huo wa kundi H ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 ulilazimika kusimamishwa katika kila kipindi huku wachezaji wakitolewa nje ya uwanja baada mwamuzi Bjorn Kuipers kusimamisha mchezo. Katika mchezo huo Antonio Candreva wa Italia na Ivan Perisic wa Croatia ndio waliofunga mabao. Timu hizo zote mbili zina alama 10 lakini Croatia wanaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Katika michezo mingine Malta ambao wameshindwa kufunga bao katika mechi zao sita zilizopita walifanikiwa kuona mwezi baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Bulgaria katika kundi hilo. Jamhuri ya Czech iliendelea kujiweka katika nafasi nzuri katika kundi A kufuatia ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Iceland huku Uturuki wao wakipata alama tatu kwa kuifunga Kazakhstan mabao 3-1. Kundi B Israel iliihenyesha Bosnia-Hercegovina na kuendelea kujikita kileleni kwa kushinda mabao 3-0.
No comments:
Post a Comment