Thursday, November 13, 2014

FIFA YAZISAFISHA URUSI NA QATAR KUHUSIANA NA TUHUMA ZA RUSHWA.

SHIRIKISHO la Soka la Duani-FIFA limezisafisha nchi za Urusi na Qatar zilizokuwa zikikabiliwa na tuhuma za rushwa wakati wa kugombea nafasi ya kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022. Katika taarifa ya shirikisho hilo imedai kuwa hakuna mahali popote ambapo nchi hizo zilionekana kukiuka sheria yeyote au kuwepo suala la rushwa hivyo kumaanisha walishinda kihalali katika uchaguzi uliofanyika Desemba 2010. Hata hivyo FIFA imekituhumu Chama cha Soka cha Uingereza-FA kwa kukiuka sheria wakati wa kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya kuandaa michuano hiyo mwaka 2018. FA wanatuhumiwa kwa kujaribu kumpendelea makamu wa zamani wa rais wa FIFA Jack Warner ambaye alijiuzulu wadhifa wake huo kutokana na tuhuma za ufisadi. Urusi ilishinda kupata haki za kuandaa michuano hiyo ya mwaka 2018 mbele ya Uingereza, Uholanzi, Ubelgiji, Hispania na Ureno huku Qatar wao wakishinda kuwa wenyeji wa michuano ya mwaka 2022 mbele ya Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani

No comments:

Post a Comment