Tuesday, November 11, 2014

LARSSON ATWAA MIKOBA YA KUINOA HELSINGBORGS.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Celtic, Henrik Larsson amejiuzulu nafasi yake ya ukocha katika timu ya Flalkenbergs na kuchukua mikoba ya kuinoa Helsingborgs ambayo aliwahi kuichezea kwa vipindi viwili tofauti. Larsson mwenye umri wa miaka 43, ambaye amewahi kuichezea Sweden mechi 106, aliwahi kuichezea Helsingborgs mwaka 1992-1993 na kati ya mwaka 2006 na 2009. Nyota huyo ambaye alishinda mataji manne ya Ligi Kuu nchini Scotland akiwa na Celtic, Mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Barcelona anachukua mikoba ya kuinoa timu hiyo ambayo imemaliza katika nafasi ya tisa katika msimamo wa Ligi Kuu nchini Sweden msimu huu. Helsingborgs ambao walishinda taji lao la tano katika ligi ya nchi hiyo mwaka 2011, wamekuwa wakifunikwa na mahasimu wao Malmo ambao wameshinda mataji mawili ya ligi mfululizo. Kikosi chao kinamjumuisha mtoto wa kiume wa Larsson mwenye umri wa miaka 17 aitwaye Jordan ambaye naye ni mshambuliaji aliyejiunga na klabu hiyo Julai mwaka jana.

No comments:

Post a Comment