Thursday, November 13, 2014

NEYMAR, MESSI WAZIONGOZA NCHI ZAO KUSHINDA.

WACHEZAJI nyota wa Barcelona, Neymar na Lionel Messi wote wamefunga mabao wakati Brazil na Argentina zilipoibuka na ushindi katika michezo yao ya kirafiki ya kimataifa jana lakini Uholanzi wao waliteleza tena kujikuta wakichapwa. Jijini Instabul, Brazil ilifanikiwa kuigaragaza Uturuki kw mabao 4-0 ambapo kocha Dunga alisheherekea ushindi wake wa tano mfululizo toka achukue mikoba ya kuinoa timu hiyo kwa mara nyingine. Katika mchezo huo Neymar alifunga mabao mawili katika dakika ya 19 na 60 huku mengine yakifungwa na Willian katika dakika ya 44 na moja la kujifunga lililowekwa kimiani na Semih Kaya. Kwa upande wa Argentina wao walifanikiwa kutoka nyuma na kuichabanga Croatia kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa jijini London kwa mabao yaliyofungwa na Cristian Daniel Ansaldi katika dakika ya 49 na Messi aliyefunga kwa njia ya penati katika ya 57. Huko Amsterdam hali imezidi kuwa mbaya kwa Uholanzi baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Mexico huku zikiwa zimebaki siku nne kabla ya mchezo muhimu wa kufuzu michuano ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya Latvia hatua ambayo inaweza kupelekea kocha Guus Hiddink kujiuzulu kama wakifungwa tena. Mechi zingine za kirafiki zilizochezwa jana ziliwakutanisha Ubelgiji walioifunga Iceland kwa mabao 3-2 na Estonia wao waliichapa Norway kwa bao 1-0.

No comments:

Post a Comment