MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger ana uhakika kuwa mashabiki wa timu hiyo watarajie kuona ubora wa Mesut Ozil wakati atakaporejea kutoka katika majeruhi yanayomsumbua. Nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani kwasasa anajiuguza goti lake aliloumia akiwa katika majukumu ya kimataifa huku akitarajiwa kurejea tena uwanjani mapema mwakani. Ozil amekuwa akikosolewa kwa kucheza kwa kiwango cha chini katika wiki za mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ingawa Wenger alifafanua suala hilo kuwa linatokana na uchovu baada ya Ujerumani kunyakuwa Kombe la dunia nchini Brazil. Wenger amesema Ozil alicheza vyema akiwa nao msimu uliopita lakini msimu huu uchovu wa Kombe la Dunia umemfanya kushindwa kuonyesha makali yake yaliyozoeleka. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa mashabiki wasiwe na wasiwasi kwani ana uhakika Ozil atarejea akiwa na nguvu mpya na katika ubora wake uliozoeleka. Arsenal kwasasa wanashikilia nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa wameshinda mechi nne pekee kati ya 11 walizocheza hivyo kuwafanya kuzidiwa na vinara Chelsea kwa alama 12.
No comments:
Post a Comment