Wednesday, November 5, 2014

RAIS WA LE HARVE AMKINGIA KIFUA ADRIANO.

RAIS wa klabu ya Le Harve inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa, Jean-Pierre Louvel amesema kesi ya madawa iliyofunguliwa dhidi ya Adriano haitabadilisha msimamo wao wa kumsajili mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Brazil. Waendesha mashitaka nchini Brazil wamemtaka nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 kusalimisha hati yake ya kusafiria baada ya kuhusishwa na mmoja wa vigogo wa madawa ya kulevya nchini humo jana. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Inter Milan anatuhumiwa na polisi kununua pikipiki mwaka 2008 ambayo ilikuwa ikitumiwa na mtandao wa madawa ya kulevya katika kundi lenye maskani yake jijini Rio de Janeiro. Louvel aliwaambia wana habari baada ya tuhuma hizo kuwa haoni kama kutakuwa na tatizo lolote kwani matatizo yalifanyika kipindi cha nyuma na Adriano alishakiri kufanya makosa hayo kwa bahati mbaya. Adriano ambaye ameitumikia Brazil katika mechi 18, amewahi kushinda mataji manne ya Serie A akiwa na Inter.

No comments:

Post a Comment